Je Ellen G. White alifundisha Kristo ni nani?

Je Ellen White aliamini nini kuhusu Yesu? Je alifundisha kwamba Yesu ndiye Mungu Baba Mwenyezi au Mwana wa Mungu? Leo inaaminiwa miongoni mwa Waadventista wengi, kwa mjibu wa fundisho la utatu kwamba Mwana na Baba ni Mungu mmoja tu yuleyule, kwamba Yesu hayupo Yeye kama Yeye Binafsi, bali Yesu na Mungu ni mtu mmoja tu na wala si watu wawili.

Imani hii imeingia kanisani kuanzia mwaka 1981, Waadventista wa awali wote hawakuamini fundisho la utatu kwa sababu haliwezi kuthibitishwa kutoka katika Maandiko. Waadventista wengi wanakubali kwamba Ellen G. White alikuwa nabii wa kweli, lakini Ellen White kamwe hakufundisha fundisho la utatu.


1). Je Ellen White alifundisha kwamba Yesu na Mungu ni mtu mmoja au wawili?

“Kristo ni umoja na Baba, lakini Kristo na Baba ni Nafsi mbili tofauti.”–(Ellen G. White, RH June 1, 1905).

Sio tu kwamba Ellen White ndiye anafundisha kwamba Yesu na Baba ni watu wawili tofauti, Biblia yenyewe inafundisha ukweli huu. Angalia jinsi inavyosema Yesu na Mungu ni watu wawili!

Zekaria 6:13 “…na kutakuwa na kuhani [Yesu] katika kiti chake [Mungu] cha enzi; na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili.”

Hivyo kulingana na Biblia na Ellen White, wote wanafundisha kwamba Kristo na Mungu ni watu wawili tofauti, na sio mtu mmoja kama fundisho la utatu linavyosema.


2). Biblia na Ellen White wote wanafundisha kwamba Yesu ni Mungu kweli! Je hii inamaanisha nini? Je Ellen White alifundisha nini kuhusiana na Uungu wa Yesu Kristo?

“Bwana Yesu Kristo, Mwana mzaliwa pekee wa Baba, kiukweli ni Mungu katika kutokuwa na ukomo, lakini sio katika nafsi.”–(Ellen G. White, Upward Look, p. 367).

Je umeshika hapo? Ellen White anafundisha kwamba Yesu ni Mungu, lakini sio Mungu katika nafsi ya Mungu. Yesu ni Mungu kwa sababu ni Mwana halisi wa Mungu ambaye alirithi asili ya kiungu kutoka kwa Baba yake, lakini Yeye siye Mungu Mwenyewe ambaye ni Baba yake. Kufundisha kwamba Mwana na Baba wote ni mtu na Mungu mmoja tu, ni sawa na kusema kwamba, kwa sababu mimi ni mwanadamu na baba yangu ni mwanadamu basi mimi na baba ni mtu na mwanadamu mmoja tu kitu ambacho hakina mantiki kabisa.

Sio tu kwamba Ellen White pekee ndiye anafundisha kwamba Yesu ni Mungu lakini sio Mungu katika nafsi ya Mungu Baba yake, Biblia yenyewe inafundisha ukweli huuhuu.

Yohana 1:1 “Hapo mwanzo kulikuwako neno, naye neno alikuwako kwa Mungu, Naye Neno alikuwa Mungu”

Je umeshika hapo? Biblia inaeleza wazi kabisa kama vile mchana kwamba Neno ni Mungu, lakini Yuko kwa Mungu. Neno anayetajwa hapa ni Yesu (angalia aya 14). Hii inamaanisha kwamba Yesu ni Mungu lakini yuko kwa Mungu ambaye ni Baba yake. Ukweli uko wazi sana kwamba Yesu ni Mungu, lakini Yesu sio Mungu katika nafsi ya Mungu, yaan, Yesu sio Mungu katika utambulifu au uelewa wa kumrejea “Mungu Mwenyezi Mwenyewe”, lakini Uungu wake Yesu unatokana na kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu, na hivyo alirithi asili ya kiungu kutoka kwa Baba yake. Ni wale tu wanaojikinai na kuishia kudharau ndio watashindwa kuitambua maana halisi ya uungu wa Yesu.


3). Kama Biblia na Ellen White wote wanafundisha kwamba Yesu ni Mungu kabisa, lakini siyo Mungu katika nafsi ya Mungu Mwenyewe, basi ni lazima pia wafundishe kwamba Yesu siyo Mungu Mwenyezi.

“Mtu Kristo Yesu hakuwa Bwana Mungu Mwenyezi, lakini Kristo na Baba ni umoja.”–(Ellen G. White, SDA Bible Commentary, vol 5, p 1129).

Sasa umeona kwamba Yesu sio “Bwana Mungu Mwenyezi”? Sababu kuu ambayo Ellen White anaandika ukweli huu ni kwamba Yesu katika agano la kale alijulikana kama “malaika wa Bwana”, na kwa jina hili Yesu alimtokea Musa katika mwali wa moto (Kutoka 2:3), pia aliwatokea na wazee na manabii wote wa zamani. Kama ukisoma maeneo yote ya Agano la kale ambapo “malaika huyu wa Bwana alitokea”, utagundua kuwa malaika huyu ameitwa majina mbalimbali, wakati mwingine ameitwa Mungu, wakati mwingine Bwana Mungu au Bwana (Yehova) n.k.

Kwa mfano; angalia kwa makini katika Kutoka 2:3 ambapo malaika huyu alimtokea Musa katika mwali wa moto, na malaika huyu alipoanza kuzungumza na Musa, baadaye katika mafungu yanayofuata 4-6 ametajwa kama Bwana, Bwana Mungu, na Mungu.

Biblia inathibitisha wazi wazi kama mchana kwamba malaika huyu aliyemtokea Musa katika mwali wa moto alikuwa ni Yesu Kristo Mwenyewe, na sababu kwanini malaika huyu katika mafungu yanayoendelea 4-6 amerejewa kama “Bwana Mungu” au “BWANA” (Yehova) inaonekana wazi katika Kutoka 23:20,21 ambapo Mungu Baba Mwenyewe anasema “JINA LAKE limo ndani ya malaika wake” ambaye ni Yesu Kristo. Na hivyo malaika huyu ambaye ni Yesu Mwenyewe, kuitwa BWANA au Bwana Mungu, ilikuwa ni kwa sababu JINA LA MUNGU (YEHOVA) lilikuwa ndani yake. Na Ellen White anaonyesha wazi wazi kwamba Yesu hakuwa Bwana Mungu Mwenyezi, ingawa kama “malaika wa Bwana” wakati mwingine aliitwa hivyo; BWANA au Bwana MUNGU.

Kwa sababu Yesu ni Mwana halisi wa Mungu, na alirithi vitu vyote kutoka kwa Mungu (Waebrania 1:2,3), pamoja na jina lililotukuka kupita la malaika wote (aya 4), pia akapewa na mamlaka yote mbinguni na duniani (Mathayo 28:18), hivyo ilikuwa ni haki Yesu atumie jina YEHOVA la Baba yake.

Kwa mfano; mimi naitwa “Jackson,” baba yangu anaitwa “Kayanda”, baba yangu akiwa hai na mimi nikali ni hai, mimi pia nikiwa kama mrithi wa vitu vyote alivyo navyo baba, kama ikitokea baba yangu akanituma kwenda kusimamia au kuangalia miradi na mali zake lazima nitatumia jina la baba mwenyewe, na watu wote katika eneo hilo wataniita “kayanda” jina la baba; kwa maana mimi nitakuwa mwenye mamlaka yote, uamuzi wote, na nitapewa heshima moja kama ile anayopewa baba yangu; kwa maana mimi ninamwakilisha kikamilifu baba yangu mwenyewe. Pia kama baba aliitwa “bosi”, “bwana”, “mkuu”, au “mzee”, mimi pia nitaitwa vivyo hivyo kana kwamba hakuna utofauti kati yangu na baba. Lakini hii haitamaanisha kwamba kwa sababu mimi natumia jina la baba, basi mimi na baba ni mtu mmoja tu yuleyule. Hapana! Mimi na baba tuko watu wawili halisi ingawa tunatumia jina moja; mimi ni “mwana” na yeye ni “baba”; yeye ni mkuu kuliko mimi katika maana ya muda pia kwa sababu yeye ni baba na mimi ni mwana. Mimi na yeye tuna usawa mmoja na sifa moja na asili moja; kwa sababu yeye ni mwanadamu na mimi ni mwanadamu, na mali zake, nguvu zake, na vitu vyake vyote ni vyangu. Yeye ni mkuu kwa maana ya kwamba yeye ni wa kwanza, na ni chanzo cha kuwepo vitu vyote, wakati mimi ni mmiliki, msimamizi, muongozaji, mtawala, n.k., wa vitu vyake vyote. Vitu vyake vyote ni vya kwangu, mamlaka hayo ninayo si kwa sababu nimependelewa au nimemwibia baba. Hapana! Bali ni kwa sababu hiyo ni halali na ni haki yangu kama mwana. Maana baba mwenyewe anapenda niwe hivyo, kwa sababu wakati wote ninafanya yale tu yanayompendeza. Hivyo ndivyo Yesu na Mungu walivyo.

Hakuna ukamilifu kwa wanadamu na kazi zao zote, lakini pia hakuna kutokamilika upande wa Mungu na kazi zake zote, na hivyo mfano wa kibinaadamu ni mdogo tu ili kuaksi sifa halisi zilizo kuu kati ya Yesu na Mungu.


4). Kwa sababu Biblia na Ellen White wanafundisha kwamba Yesu ni Mungu kabisa, lakini sio Mungu katika nafsi ya Baba, basi ni lazima pia wafundishe kwamba Yesu ni Mwana halisi wa Mungu na Mungu ni Baba halisi wa Yesu, na kwa sababu hiyo Uungu wa Yesu utakuwa; ni Mungu kwa sababu ni Mwana wa Mungu, kama wewe ulivyo mwanadamu kwa sababu u mwana wa mwanadamu.

“Maandiko yanaonyesha wazi wazi uhusiano kati ya Mungu na Kristo, na yanaleta kwenye wazo kama ilivyo wazi Nafsi na Nafsi ya kila mmoja [Waebrania 1:1-5 imenukuuliwa]. Mungu ni Baba wa Kristo; Kristo ni Mwana wa Mungu. Kwa Kristo imetolewa nafasi iliyotukuka. Amefanywa sawa na Baba. Makusudi yote ya Mungu yamefunguliwa kwa Mwana wake.”–(Ellen G. White, Testimonies for the Church, vol 8, p 268).

Unataka niorodheshe mamia ya mafungu yote yanayosema Yesu ni Mwana wa Mungu na Mungu ni Baba wa Yesu? Yatajaza kurasa na kurasa! Haya hapa ni machache tu kati ya mamia yanayosema wazi kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu na Mungu Ni Baba wa Yesu.

Miongoni mwa mashahidi wote, shahidi aliye mkuu kuliko wote ni Baba wa mbinguni. Zaidi ya mara moja aliongea kutoka mbinguni kwamba “Huyu ni Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye.” Mathayo 3:17; 17:5.

Yesu Mwenyewe alitangaza kwamba, “Mimi ni Mwana wa Mungu” Yohana 10:36. Akasema zaidi kwamba, Yeye ni “Mwana mzaliwa pekee wa Mungu.” Yohana 3:16,18.

(Bofya hapa kupata mamia ya mafungu yanayomwita Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu)


5). Kama Ellen White anafundisha kwamba Yesu na Mungu ni watu wawili halisi kama Biblia inavyothibitisha pia, na Ellen White alikuwa ni nabii, Je alipewa maono kuhusu Yesu?

“Mara kwa mara nimekuwa nikimwona mpendwa Yesu kwamba Yeye ni nafsi. Nilimuuliza kama Baba yake naye ana nafsi na ana umbo kama yeye mwenyewe. Alisema Yesu, “Mimi niko katika mfano wa nafsi ya Baba yangu.” Mara kwa mara nimeona kwamba wazo la umizimu huchukulia mbali utukufu wote wa mbinguni […].” –(Ellen G. White, Early Writtings, p 77).

Angalia jinsi Ellen White anasema alimwona Yesu akiwa peke yake, na Yesu akasema “Yeye ni mfano wa Baba yake”. Ellen White anaongeza kuwa wazo la kusema kwamba Yesu na Baba ni mtu mmoja tu yuleyule ni wazo la UMIZIMU na linaharibu utukufu wote wa mbinguni! Angalia Ellen White jinsi anavyosikitika kiasi gani watu ambao wameujua ukweli wa kiadventista walivyoongozwa kuamini fundisho la utatu wazo la umizimu.

“Baada ya kupita wakati wa mwaka 1844, tulikuwa na ushabiki wa kila aina kukutana nao. Shuhuda za maonyo zilikabidhiwa kwangu ili kuzipeleka kwa baadhi ya watu wanaoshikilia nadharia za kiumizimu. Kulikuwa na wale ambao wako hai katika kusambaza mawazo ya uongo kuhusu Mungu. Nuru ilitolewa kwangu kwamba watu hawa walikuwa wanafanya ukweli usio na faida kwa mafundisho yao ya uongo. Niliagizwa kwamba walikuwa wanapoteza nafsi za watu kwa kuleta nadharia za kubahatisha kuhusu Mungu.” –(Ellen G. White, Testimonies, vol 8, p 292, 293. 1904).

Sasa kama umesoma hii unajua Ellen White siku zote anayahusisha mafundisho ya uongo kuhusu Mungu kama “umizimu”. Zingatia nukuu ifuatayo; maana ni ya muhimu kwa Waadventista wote walioongozwa kuamini mafundisho ya utatu.

“Ni jambo ambalo haliwezi kuchukuliwa kama jambo dogo kwamba watu ambao wamekuwa na nuru kuu sana, na ushahidi ulio wazi kama uhalisi wa ukweli tunaoshikilia, wangekuja kuhangaishwa na kuongozwa kukubali nadharia za kiumizimu kuhusu nafsi ya Mungu.” –(Ellen G. White, Special Testimonies, Series B7, p 37).

Sasa unajua wazi kwamba Ellen White anasema umizimu ni mafundisho ya uongo kuhusu Mungu, na zaidi anasema wale wanaokataa kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu na Mungu ni Baba wa Yesu wanaamini umizimu na ndio wapinga Kristo.

“Umizimu wa siku hizi, umetulia juu ya msingi uleule, ni uhuikaji katika mfumo mpya wa uchawi na ibaada ya pepo ambayo Mungu aliikataza zamani…Petro akielezea hatari ambazo zingekuja kanisani katika siku za mwisho, anasema kwamba kama vile kulivyokuwako manabii wa uongo ambao waliiongoza Israeli katika dhambi, hivyo hivyo kutakuwako na walimu wa uongo, “wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na wengi watafuata ufisadi wao” 1Petro 2:1, 2. Hapa mtume Petro ameonyesha moja ya tabia za waalimu wa umizimu. Wanakataa kumkubali Yesu kama Mwana wa Mungu. Kuhusu walimu kama hao mpendwa Yohana anasema wazi; “Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.” 1Yohana 2:22, 23. Umizimu, kwa kumkataa Kristo, wamewakataa wote Baba na Mwana, na Biblia inatangaza wazi udhahiri huu kuwa ni upingaKristo.” –(Ellen G. White, Patriarchs and Prophets, p 686).

Sio Ellen White peke aliyefundisha kwamba kukataa kwamba Yesu ni mtu mmoja anayejitegemea tofauti na Baba yake ni umizimu na upingakristo, waasisi wote wa SDA walitambua fundisho la utatu ni umizimu kwa kuwa linamkana Kristo kama Mwana wa Mungu. Angali James S. White mume wa Ellen G. White, anavyoeleza.

“Jinsi ambavyo wanaumizimu wamemwacha au kumkataa Bwana Mungu pekee na Bwana wetu Yesu Kristo kwanza ni kwa kutumia imani ya utatu mtakatifu isiyo ya kimaandiko, kwamba Yesu Kristo ni Mungu wa Milele, na ujue hawana hata fungu moja la kuunga mkono jambo hilo, wakati tuna ushuhuda ulio wazi wa Maandiko mengi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu wa milele.” –(James White, The Day Star, Jan. 24, 1846).

Sio tu kwamba Ellen White ndiye anafundisha kwamba, utatu ni umizimu na upinga Kristo, Biblia yenyewe inasema wazi kwamba kukataa kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu huu ni upingaKristo.

1 Yohana 2:22-23 “Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.”

“Wale ambao huchanganyikiwa katika uelewa wao wa neno, ambao hushindwa kuiona maana ya mpinga-Kristo, kwa hakika watajiweka wao wenyewe upande wa mpinga-Kristo.” —(Ellen G. White, Seventh-day Adventist Bible Commentary, vol. 7, 949)

“Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; [lakini] amkiriye Mwana anaye Baba pia. [Par 17]…Yeye akanaye nafsi ya Mungu na ya Mwanawe Yesu Kristo, anamkana Mungu na Kristo. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba.” —(Ellen G. White, Review and Herald, March 8, 1906, p. 9)


6). Kama Ellen White alifundisha kwamba Kristo na Baba ni watu wawili tofauti, na kwamba Kristo ni Mwana wa Mungu, lazima pia afundishe kwamba Kristo siyo Mungu Baba! Lakini hata hivyo fundisho la utatu hudai kwamba Kristo na Baba ni mtu na Mungu mmoja tu, hii inamfanya Kristo kuwa Baba na Baba kuwa Kristo! Je Ellen White alifundisha nini kuhusu hilo? Je alifundisha kwamba Kristo ni Mungu Baba kama imani ya utatu inavyodai?

“Asili ya kiungu katika nafsi ya Kristo haikubadilishwa katika asili ya kibinadamu na asili ya kibinadamu ya Mwana wa Mtu haikugeuzwa katika asili ya kiungu, lakini kwa maajabu zilichanganywa katika Mwokozi wa watu. Yeye hakuwa Baba bali katika yeye ulikaa utimilifu wote wa Uungu kwa jinsi ya kimwili,” —(Ellen G. White, Letter 8a, July 7, 1890)

Ni wazi kabisa Ellen White alifundisha kwamba Kristo siyo na wala hakuwa Mungu Baba. Biblia inafundisha wazi kabisa kwamba Kristo siyo Mungu Baba, mara kwa mara Yesu anasema, “Baba yangu aliye mbinguni”, na Baba Mwenyewe zaidi ya mara moja amemwita Yesu akiwa duniani “Mwanangu ninayependezwa naye” (Mt. 3:17; 17:5).

Wakati wa ubatizo wa Yesu tunaona nafsi tatu zote za uungu zinaonyeshwa wazi, Yesu alikuwa duniani anapanda kutoka katika mto Yordani, Baba alikuwa juu mbinguni akimshuhudia Yesu kuwa Mwanaye anayempenda sana, na Roho Mtakatifu (utukufu wa Mungu uliokuwa katika umbo kama la njiwa) alikuwa angani anashuka kuja juu ya Yesu. Hapa ilikuwa wazi sana kwamba Baba ni mtu mmoja pekee aliyekuwa mbinguni, wakati Yesu naye ni mtu pekee aliyekuwa duniani (angalia Mathayo 3:15-17).

Tena katika sala ya Yesu bustanini, Yesu alimwomba Baba yake aliye mbinguni “ikiwezekana kikombe kimwepuke” Mt 26:39. Kama Yesu alikuwa ndiye Mungu mmoja Baba, ingewezekanaje aombe kuondoshewa kikombe na Baba mwingine? Hii pekee ingemfanya Yesu kuwa muongo; kwa maana Yeye mwenyewe ni Baba lakini anaomba kwa Baba mwingine ikiwezekana kikombe kimwepuke. Wakati Yesu anakata roho pale msalabani, “akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Luka 23:46-47. Je roho yake ingeenda mikononi mwa nani kama Yeye mwenyewe alikuwa ndiye Baba? Pia 1 Timotheo 6:16 inasema Baba hawezi kufa kwa namna yoyote, Je Yesu aliwezaje kufa kama alikuwa ni Baba? Baada ya kufufuka katika Mathayo 28:18 Yesu akawaambia wanafunzi wake kwamba “nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”. Je mamlaka hayo aliyapewa na nani kama Yeye ni Baba? Hatimaye katika Waebrania 1:3,4 tunaambiwa kwamba “Yesu amerithi vitu vyote vya Mungu”. Je anawezaje kurithi ikiwa Yeye ndiye Mungu mmoja Baba? Hii kwa wazi inaonyesha Yesu ni Mtu mwingine tofauti na Baba.

Hata hivyo, kwa sababu ushahidi uliotolewa hapo juu unaonyesha haiwezekaniki Yesu kuwa Baba, wanautatu wamekuja na nadharia kwamba Yesu alikuwa na “asili mbili”; ya kibinaadamu na ya kiuungu. Wanasema kwamba asili ya kibinaadamu ndiyo ilikufa msalabani lakini Yesu Mwenyewe kama Mungu mmoja Baba hakufa msalabani. Kama hii ni kweli, basi yule aliyefufuka naye alikuwa ni mwanadamu tu, na yule aliyepewa mamlaka yote mbinguni na duniani naye alikuwa ni mwanadamu tu, na yule aliyerithi vitu vyote vya Mungu naye ni mwanadamu tu. Ndiyo! Kwa maana kama Yesu ni Mungu Mmoja Baba, yeye hawezi kufa, kufufuka, kurithi, wala kupewa mamlaka, hii itamaanisha kuwa yule anayepewa mamlaka katika Mathayo 28:18 siyo Yesu bali ni mwanadamu tu, na yule anayerithi vitu vyote vya Mungu katika Ebr. 1:3,4 siyo Yesu bali ni mwanadamu tu. Na hivyo katika fundisho la utatu kuna Yesu mwingine bandia ambaye hana asili ya kiuungu, bali ni mwaanadamu tu ambaye anahubiriwa kwa siri.


7). Wanautatu ili kuthibitisha rasmi fundisho lao kwamba Yesu ni Mungu mmoja Baba, wanatumia Yohana 10:30 ambapo Yesu alisema, “Mimi na Baba tu umoja.” Lakini Je Ellen White alifundisha nini kuhusu umoja wa Yesu na Baba?

“Umoja uliopo kati ya Kristo na wanafunzi wake hauharibu nafsi aidha. Wao ni wamoja katika lengo, katika akili, katika tabia, lakini si katika nafsi. Ni kwa hivyo kwamba Mungu na Kristo ni umoja.” —(Ellen G. White, 8T 269.4, 1904)

Ellen White anaonyesha wazi kwamba umoja wa Yesu na Baba ni kama umoja wa Yesu na wanafunzi wake, umoja wao haumaanishi kwamba wote ni Mtu na Mungu mmoja tu, bali unamaanisha kwamba wana nia, lengo na tabia moja tu.

Kuhusu umoja wa wanafunzi Paulo anasema, “Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.” Rum 12:5. Kama Wakristo wote ni “mwili mmoja”, Je hii inamaanisha kwamba Wakristo wote wanayeyuka na kuwa Mkristo mmoja tu? Kwa hakika hapana! Sasa angalia jinsi Yesu anavyoeleza kwamba umoja wa wanafunzi ni kama umoja wake Yeye na Baba.

Yohana 17:11 inasema, “Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.”

Yohana 17:22 “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.”

Sasa kama umoja wa Yesu na Baba unamaanisha wao ni Mtu na Mungu mmoja tu, pia wanafunzi wa Yesu wote wangekuwa ni mtu na mwanafunzi mmoja tu; kwa maana wote wana umoja sawa. Lakini umoja wa wanafunzi sio wa kuyeyuka na kuwa mtu mmoja, ni vivyo hivyo umoja wa Yesu na Baba. Yesu ni mtu mmoja pekee, na Baba ni mtu mmoja pekee, umoja wao ni uelewano uliopo kati yao.


Advertisements

Comments are closed.

%d bloggers like this: