Je Mitume walitunza Sabato ya Jumamosi au Jumapili? Biblia na Historia: Sehemu ya 2.


Rudi: Sehemu ya 01


Paulo na Sila waanzisha kanisa huko Filipi la watunza Sabato, ya Jumamosi!

Baada ya Paulo na Barnaba kushindana, Barnaba alienda pamoja na Yohana, wakati Paulo alienda pamoja na Sila (Mdo 15:37-40). Paulo na Sila wakapitia Shamu na Kilikia, Derbe na Listra ambapo walimpitia Timotheo, kisha wakasafiri kwenda nchi ya Frigia na Galatia, wakapitia Misia, na Bithinia, na Troa ambapo Paulo alipata maono akiambiwa avuke kwenda Makedonia, na kutoka hapo wakasafiri hadi Samothrake na Neapoli; na kutoka hapo wakafika Filipi mji mkuu wa jimbo la Makedonia.

Matendo 16:12 “na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha.”

Paulo akiwa na Sila na Timotheo pamoja na Luka mwenyewe ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Matendo, walipofika Filipi walikaa hapo siku kadhaa. Je Paulo alitunza Sabato huko Filipi au alitunza Jumapili? Angalia Luka mwenyewe ambaye alikuwa pamoja na Paulo huko Filipi jinsi anavyoshuhudia:

Matendo 16:13 “Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.”

Kwanini walitoka nje kutafuta mahali pa kusali siku ya Sabato, kama Yesu angekuwa ameigeuza siku ya kusali, na kama ufufuo wake na siku ya Pentekoste viliingiza Jumapili? Kwanini hawakusubiri Jumapili ili kwenda kutafuta mahali pa kusali, badala yake wakafanya hivyo siku ya Sabato? Ilikuwa ni desturi ya Paulo kwenda kwenye sinagogi kila siku ya Sabato ili kusali, lakini katika Filipi hapakuwa na sinagogi, hata hivyo Paulo na wenzake walitafuta mahali pa kwenda kusali. Je hiyo ingewezekanaje kama Sabato ilikuwa imetanguka? Kwa hakika Paulo, Timotheo, Luka pamoja na Sila wote walikuwa Wasabato, hakuna mahali popote katika Biblia panaposema kwamba Paulo alienda katika sinagogi siku ya Jumapili. Na kwa kuwa huko Filipi palikuwa hakuna sinagogi, hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya Paulo kusali siku ya Jumapili, lakini hakufanya hivyo, bali siku ya Sabato akatafuta mahali pa kusali. Hauwezi kusema kwamba Paulo alitunza Jumapili, au kwamba makanisa yote ambayo aliyaanzisha yalitunza Jumapili. Makanisa yote aliyoanzisha Paulo ni ya watunza Sabato kama yeye mwenyewe alivyo mtunza Sabato.

Sasa Paulo na wenzake walipokuwa wakitafuta mahali pa kusali, walikusanyika pamoja na wanawake kadhaa wa mji huo; ambapo mwanamke mmoja anayeitwa Lidia, alikuwa ameandaliwa na Bwana ili ayatunze maneno ya Paulo. Baadaye mwanamke huyo alibatizwa pamoja na nyumba yake, na Paulo na wenzake wakaendelea kuishi huko kwa muda mrefu, huku kila Sabato walikusanyika kusali mahali pale.

Matendo 16:16 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. 17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.”

Kijakazi huyo mwenye pepo aliendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu hadi Paulo akaamua kumkemea yule pepo naye akamtoka, kitu kilichoamsha hasira za mabwana wa kijakazi huyo; maana walijipatia pesa nyingi kupitia kijakazi huyo mwenye pepo aliyekuwa akiagua, wakawakamata Paulo na Sila na kuwashitaki kwa uongo mbele ya watu wa mji, nao wakawapiga bakora na kuwatia gerezani. Paulo na Sila walipokuwa wakiomba wakati wa usiku, lilitokea tetemeko na milango ya gereza ikafunguka. Mlinzi wa gereza alipoamuka na kuona milango iko wazi, alitaka kujiua lakini Paulo akamzuia, ndipo yule mlinzi akaongoka na familia yake nao wakabatizwa. Paulo na Sila walipata neema ya kutoka gerezani, wakaenda nyumbani mwa Lidia, wakawafariji Waumini wote kisha wakaenda zao katika mji mwingine.

Mtendo 16:40 “Nao wakatoka gerezani wakaingia nyumbani mwa Lidia; na walipokwisha kuonana na ndugu [Wakristo waliokuwa wameamini] wakawafariji, wakaenda zao.

Paulo na Sila walikuwa wameanzisha kanisa linalotunza Sabato nyumbani mwa Lidia huko Filipi, na wakati wanaondoka kutoka Filipi hawakuagiza popote kwamba waumini wa kanisa waanze kutunza Jumapili. Ni ukweli usioweza kukataliwa kwamba kanisa la huko Filipi walikuwa watunza Sabato na waliendelea kutunza Sabato kipindi chote walichoishi mitume.


Paulo na Sila waanzisha kanisa huko Thesalonike la watunza Sabato!

Baada ya Paulo na Sila wakiwa pamoja na Timotheo na Luka, kutoka Filipi “Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi.” Matendo 17:1. Je Paulo alifanya nini hapo Thesalonike siku ya Sabato?

Matendo 17:2 “Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu, 3 akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo.”

Kwanini Paulo alisubiria Sabato ndipo akahubiri habari za Kristo? Kama Jumapili ilikuwa imetakaswa, Kwanini baada ya Sabato kesho yake Jumapili asingehojiana nao kwenye sinagogi tena? Lakini alihojiana nao sabato ya kwanza, jumapili hakuhojiana nao, akahojiana nao sabato ya pili, jumapili hakuhojiana nao, tena akahojiana nao sabato ya tatu, lakini jumapili hakuhojiana nao. Na watu wengi waliamini kwa mahubiri yake aliyofanya katika sabato tatu, nao wakamfuata:

Matendo 17:4 “Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache.”

Wayahudi walipoona watu wameiamini Injili inayohubiriwa na Paulo wakajaa wivu na kuleta vurugu, bali wakristo walioamini walimtorosha Paulo usiku kwenda mji mwingine.

Matendo 17:10 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.”

Kumbuka Paulo na Sila walikuwa tayari wameacha kanisa huko Thesalonike ambalo watu walikuwa wanatunza Sabato. Na Paulo hakuacha amewaagiza popote kwamba waache sabato na kutunza jumapili! Ni ukweli usioweza kupingika kwamba kanisa la Thesalonike walikuwa watunza sabato katika kipindi chote cha mitume.


Je Yesu alitabiri kwamba mitume wangetunza Sabato katika maisha yao yote

Ushahidi mkuu ambao hauwezi kupingwa kwa vyovyote, unatoka katika kinywa cha Yesu Mwenyewe; ambapo alionyesha kuwa katika mwaka 70; hiyo ni miaka 40 baada ya Yesu kupaa mbinguni; mitume walikuwa wakitunza Sabato ya Jumamosi.

Wanafunzi wake Yesu walimuuliza kwamba: “Tuambie, mambo hayo (ya kuangamizwa kwa hekalu la Yerusalemu) yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?” Mathayo 24:3. Wakati Yesu anawajibu, alitoa ushahidi kwamba wakati wa kuangamizwa kwa hekalu la Yerusalemu mitume wangekuwa wakitunza Sabato. Yesu Akasema:

Mathayo 24:15 “Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), 16 ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;”

Mathayo 24:20 “Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.”

Chukizo la uharibifu lililonenwa na nabii Danieli lilikuwa ni kuangamizwa kwa hekalu la Yerusalemu. Danieli (9:27) alitabiri kwamba: “Naye (Masihi) atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.”

Kwamba baada ya Masihi kuuwawa msalabani, angeikomesha sadaka na dhabihu, yaani, angekomesha utoaji wa kafara ya mnyama kwa ajili ya dhambi. Kisha mahali pake, yaani, Yerusalemu, lingesimama chukizo la uharibifu, na ghadhabu kumwagwa juu yake, kwa sababu Wayahudi walikuwa wamemkataa Mwana wa Mungu. Chukizo la uharibifu lilisimama mwaka 66 BK; ambapo Wakristo waliitambua ishara na wakakimbilia milimani, kisha ghadhabu yenyewe ilimwagwa katika mwaka 70 BK; ambapo hekalu na mji wa Yerusalemu viliharibiwa kabisa kama Yesu alivyokuwa ametabiri kwamba halitasalia jiwe juu ya jiwe katika hekalu la Yerusalemu.

Mathayo 24:1-2 “Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. 2 Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.”

“Mnamo 66BK wakati Cestius alipokuja dhidi ya mji [wa Yerusalemu], lakini bila kuelezeka alirudi nyuma, Wakristo waliigundua ishara iliyokuwa imetabiriwa na Kristo na kukimbia wakati Wayahudi 1,100,000 ilisemekana waliuwawa katika maangamizi ya kutisha ya mwaka 70BK.” –(Eusebius, Church History, book 3, chap. 5).

Yesu alipotabiri kuhusu kusimama kwa chukizo la uharibifu, na akaonyesha njia kwamba walioko Yudea wakimbilie milimani, bado anasema “ombeni kukimbia kwenu kusiwe siku ya Sabato” Mathayo 24:20. Yesu alijua kwamba mwaka 66 BK, wakati Wakristo wanakimbia kutoka Yudea kwenda milimani, isingependeza kama wangekimbia siku ya Sabato. Yesu na Baba walishirikiana katika uumbaji na wakapumzika siku ya saba, hivyo Yesu alijua vema kwamba siku ya Sabato si vizuri kukimbia vita au kufanya mambo yoyote ya usumbufu, na akawaonya kwamba “ombeni kukimbia kwenu kusiwe katika siku ya sabato”; maana sabato iliwekwa na Mungu kwa ajili ya kupumzika, na sio kukimbia vita, au kufanya kazi yoyote ya usumbufu.

Hapa Yesu anadhihirisha kuwa mwaka 66 B.K wakati Wakristo wanakimbilia milimani kutoka Yerusalemu, mitume wote na Wakristo walikuwa wanatunza Sabato; kwa maana kama wangekuwa hawatunzi sabato, kulikuwa hamna haja ya kuomba ili kukimbia kwao kusiwe katika siku ya sabato! Ushahidi huu kutoka kwenye kinywa cha Yesu Mwenyewe, unathibitisha kabisa kwamba mitume na Wakristo wote wa mwanzo walitunza sabato. Huu ni ukweli usiopingika, kanisa la kipindi cha mitume lilitunza sabato katika maisha yote ya mitume wa Bwana Yesu.


Angalia pia ushahidi katika historia.

Published by JacksonSL

My name is Jackson A Kayanda (Full name: Jackson Augustine Kayanda), born on 17th January 1995 at Samina Geita in Tanzania. Went to school for pre and first class primary standard education at Shule ya Msingi Mpomvu in Mtakuja ward in the years 2001 and 2002. After there, I moved to Shule ya Msingi Nyakamwaga in Geita where I spent my final six classes in the years 2003 to 2008. In 2012, I attended a college for auto mechanics technical courses at Kirumba Technical Training Centre (KTTC) where I won a highest Certificate level (grade one) able to perform auto mechanics engineering in both theory and practical works. I'm very interested in reading and writing, this is why I launched Sabbath Light for the good, read to share inspirational facts and ready to receive corrections either. I stay calm in Christ Jesus!