Je Yesu Kristo ni Mungu?

Neno “Mungu”, katika Maandiko limetumika kwa njia mbili tofauti. Kwanza, neno “Mungu” limetumika kumrejea Mwenyezi Mungu wa mbingu na nchi ambaye ni chanzo cha kuwapo kwa vitu vyote mbinguni na duniani. Biblia mara kwa mara imemwita kama; Mungu mmoja tu, Mungu wa pekee wa kweli, na Mola aliye peke yake. Katika akili hii, hakuna Mungu mwingine ila Yeye pekee. Lakini, Pili, neno “Mungu” katika Maandiko limetumika kumrejea mtu flani mwingine tofauti, ambaye amerithi tabia, sifa, na asili ya Uungu.

Mara nyingi Maandiko yanamwita Yesu kuwa ni “Mzaliwa wa pekee au wa kwanza wa Mungu Baba” (Ebr 1:6; Yn 1:18), na kwa kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, hivyo alirithi tabia, na sifa zilezile kama za Mungu Baba yake. Inajulikana kwa kila mmoja kuwa, kila mtoto lazima alithi asili ileile kama ya baba yake.

Kwa mfano…

  1. Mwana wa nyoka, naye ni nyoka
  2. Mwana wa simba, naye ni simba
  3. Mwana wa mbwa, naye ni mbwa
  4. Mwana wa chui, naye ni chui
  5. Mwana wa kondoo, naye ni kondoo
  6. Mwana wa mbuzi, naye ni mbuzi
  7. Mwana wa mwanadamu, naye ni mwanadamu
  8. Mwana wa Mungu, naye ni Mungu

Kwa sababu Yesu alitoka kwa Baba (Yn 16:27), neno la kigiriki lililotumika katika Yn 16:27 kwa ajili ya “nalitoka” ni “exerchomai” (ἐξέρχομαι), ambalo linamaanisha “kutoka nje ya” Baba. Hivyo, Kristo ni wa kiini kilekile cha Baba yake na hata hivyo ana asili ya Mungu ileile kama ya Baba yake kwa kuwa aliirithi kutokana na kuzaliwa na Baba, na alirithi tabia na sifa zote za Baba yake. Kwa kweli, Waebrania 1:3 inasema, “…[Kristo] ni chapa ya nafsi yake [Mungu]…”. Mwana siku zote ana haki ya kuchukua jina la baba yake, na hivyo Kristo kama Mwana wa Mungu ana haki ya kuchukua jina la Baba yake.

Waebrania 1:1-6 inasema, “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii…mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.”

Hivyo, Yesu Mwana pekee wa Mungu kama mrithi wa yote, amerithi jina lililotukuka zaidi kupita jina la malaika, na jina hilo ni jina la “Mungu”. Mtume Paulo katika Waebrania 1:8,9 anaonyesha wazi kuwa jina alilorithi Yesu kutoka kwa Baba yake ni jina la “Mungu”. Angalia jina lenye rangi ya kijani linamhusu Yesu, na lenye rangi nyekundu linamhusu Baba yake na Yesu.

Waebrania 1:8,9 “Lakini kwa habari za Mwana [Mungu] asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio.”

Hapa Mungu Baba Mwenyewe anamwita Mwanawe Yesu Kristo, kwamba ni Mungu, na tena, anaonyesha wazi kuwa japokuwa Yesu ni Mungu lakini na Yeye ana Mungu ambaye ndiye aliyemtia mafuta na ndiye Baba yake.

Hivyo, Yesu ni Mungu kwa sababu ni Mwana wa Mungu. Lakini Yeye sio na hawezi kuwa “Mungu Baba”. Yeye ni “Mwana wa Mungu” na hivyo ndivyo alivyo kama vile Biblia inavyomtaja zaidi ya mara mia. Yeye ni Mwana halisi wa Mungu. Na kama mtu akisema “Yesu ni Mungu Baba”, ni sawa na kusema “Mwana ni Baba na Baba ni Mwana” kitu ambacho kitamaanisha kwamba Mwana si Mwana kweli, na Baba si Baba kweli, lakini ni mtu mmoja tu ambaye anajifanya yeye mwenyewe kuwa Baba na Mwana kwa wakati mmoja. Au, kwa jinsi nyingine, kama mtu akisema kuwa Yesu ni Mungu Baba Mwenyewe, haitofautiani na kusema kuwa, kwa kuwa mimi ni mwanadamu na baba yangu ni mwanadamu, basi mimi ni baba yangu mwenyewe; kitu ambacho hakina mantiki yo yote kabisa.

Kwa ajili ya Waadventista: Ellen White anakubaliana na maelezo yafuatayo.

“Jina hili hakupewa Kristo katika matokeo ya baadhi ya mafanikio makubwa, lakini ni lake kwa haki ya urithi. Akizungumzia nguvu na ukuu wa Kristo, Mwandishi kwa Waebrania anasema kwamba Yeye amefanywa bora zaidi kuliko malaika, kwa sababu “Yeye kwa urithi amepata jina lililo tukufu zaidi kuliko lao.” Ebr. 1: 4. Mwana daima kihalali huachukua jina la baba yake; na Kristo, kama “Mwana pekee wa Mungu,” ana haki ya jina lilelile. Mwana, pia, kwa kiasi kikubwa au kidogo, ni, uzazi wa baba yake; yeye ana, kwa kiasi fulani, tabia na sifa binafsi za baba yake; si kikamilifu, kwa sababu hakuna uzazi kamili kati ya wanadamu. Lakini hakuna kutokamilika kwa Mungu, au kwa kazi zake zozote; na hivyo Kristo ni “chapa” ya nafsi ya Baba. Ebr. 1:3. Kama mwana wa Mungu-aliyepo binafsi, kwa asili ana sifa zote za Uungu. Ni kweli kwamba kuna wana wengi wa Mungu, bali Kristo ni “Mwana wa pekee wa Mungu,” na kwa hiyo ni Mwana wa Mungu kwa maana ile ambayo hakuna mtu mwingine aliyewahi kuwa, au anayeweza kuwa. Malaika ni wana wa Mungu, kama alivyokuwa Adam (Ayubu 38:7; Luka 3:38), kwa kuumbwa; Wakristo ni wana wa Mungu kwa kupitishwa (Rum 8:14,15); bali Kristo ni Mwana wa Mungu kwa kuzaliwa. Mwandishi kwa Waebrania zaidi anaonyesha kwamba nafasi ya Mwana wa Mungu si moja ambayo Kristo ameinuliwa, lakini kwamba ni moja ambayo Anayo kwa haki.” —(E.J. Waggoner, Christ and His righteousness, p. 11-12)

Katika Waebrania 1, fungu la 4 linasema kuwa Yesu, “amefanyika bora kupita malaika, kwa kadri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.” Harafu fungu la 8 linasema kwamba jina hili lililo tukufu zaidi ni “Mungu” ambalo Baba alimpa Mwanawe. “Kwa habari za Mwana [Mungu] asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele;” Na hivyo jina hili Yesu analo si kwa kupewa kama zawadi, lakini analo kwa kuwa ni haki yake ya urithi, na amelirithi kutoka kwa Baba yake.

Na Yesu hakurithi tu jina la Baba yake, bali alirithi na vitu vingine pia. Waebrania 1 fungu la 2 linasema kuwa Kristo, “amewekwa kuwa mrithi wa vyote.” Mrithi siku zote ni mtu mwingine anayerithi kitu kutoka kwa mtu mwingine tofauti. Na hivyo Mwana anarithi vitu kutoka kwa Baba yake. Na Je, ni vitu gani ambavyo Kristo anarithi kutoka kwa Baba? Ni jina lake, mamlaka yake, na uwezo wake. Kwa maneno mengine, Kristo kama Mwana wa pekee wa Baba, amerithi tabia zote za Mungu, na hivyo yuko sawa na Mungu, lakini Yeye ni mtu tofauti na Mungu Mwenyewe.

Hivyo, Kristo kwa kurithi jina, jina linamaanisha mamlaka(Marko 11:9, Yohana 5:43), na pia linamaanisha tabia na asili (Kutoka 33:18-19, 34:5-6). Kwa mfano; jina “Adam” ni la kiebrania linalomaanisha “mwanadamu” kwa kiswahili, na watoto wake hawarithi tu jina la “mwanadamu” bali wanarithi tabia na asili ya baba yao “mwanadamu”. Hii inamaanisha kuwa kama baba yao anakula, anaongea, analia, anacheka, anavaa, anaoga, analala, anapumua, n.k., na watoto wake wanarithi asili na tabia hizo hizo kama za baba yao, na hii ndio sababu watoto wanakuwa sawa na baba yao, lakini hawawi baba mwenyewe, na wala hawawezi kulingana na baba; kwa maana wao ni wana.

Kwa jinsi hii, Yesu amerithi kila kitu pamoja na jina kutoka kwa Mungu, na hivyo Yeye pia ni Mungu kutokana na kurithi, lakini Yeye sio Mungu Mwenyewe ambaye ni Baba, Yeye ni Mwana wa Mungu. Na kwa sababu ni Mwana wa Mungu, hivyo amerithi asili, tabia, na sifa zote kama za Mungu ambaye ni Baba yake, na hivyo Yeye yuko sawa na Mungu, lakini halingani na Mungu kabisa kwa sababu Yeye ni Mwana, na wala sio Baba. Yesu hakurithi tu jina, bali hata uhai alionao katika nafsi yake aliurithi kutoka kwa Baba yake. Yesu katika Yohana 5:25 anasema, “Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.” Hivyo, uhai alionao Kristo aliupata kutoka kwa Baba yake, uhai kiurahisi unamaanisha Roho. Na kwa sababu katika Uungu hakuna Roho mbili, bali kuna Roho mmoja tu ambaye ni Roho Mtakatifu (Waefeso 4:4), hivyo Kristo na Mungu Baba wote wana Roho moja tu ambayo huitwa Roho wa Kristo, na pia Roho wake Yeye aliyemfufua Kristo ambaye ni Baba (Warumi 8:9,11).

Hivyo, Kristo kwa sababu ni Mwana wa Mungu, alirithi Roho au Uhai kutoka kwa Baba yake, na kama uhai wa Kristo ni ule ule kama uhai wa Mungu, ndio maana Kristo na Mungu wako sawa, lakini kwa vyovyote, hawawezi kulingana kwa sababu Mungu Baba ndio chanzo chote cha uhai ulio ndani ya Kristo, tena Yeye ndio chanzo kikuu cha kuwapo vitu vyote hata kuwapo kwa Kristo Mwenyewe. Maandiko yanamrejea Mungu Baba kama “Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.” Waefeso 4:6, pia “Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.” 1Wakorinto 12:6

Kwa hiyo kama Baba ni yote katika wote na ni mkuu kuliko Mwanawe, ndipo Yesu angetuhakikishia kwamba, “naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.” Yohana 14:28. Na kama Baba ni mkuu kuliko Yesu, ndipo Yesu anafunua wazi kwamba, “Baba yangu…ni mkuu kuliko wote.” Yohana 10:29. Hii ndio maana Mungu Baba ni yote katika yote na juu ya wote.

Mungu mmoja aliye Baba ndiye chanzo cha vyote, na Yesu Kristo ni mfereji wa kupitia vitu vyote. 1Wakorinto 8:6 inasema, “Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake“, hii inamaanisha kwamba kila kitu kimetokana na Mungu Baba, hata Yesu mwenyewe. Harafu inaendelea kusema, “yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo“, Hii inamaanisha kwamba Baba ndiye chanzo kikuu cha vitu vyote, lakini ili vitu hivyo viwepo vinapitia kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu. Kwa mfano; Mungu aliuumba ulimwengu kupitia Mwanawe Yesu Kristo (Ebr. 1:2), hivyo aliyekuwa chanzo kikuu cha kuumbwa kwa ulimwengu ni Mungu Baba, lakini ulimwengu ulikuwapo kwa kupitia Kristo Mwana wake.

Ilimpendeza Mungu kwamba “katika yeye [Yesu]…utimilifu wote ukae.” Wkolosai 1:19, hivyo Yesu akapewa mamlaka yote, lakini usisahau kwamba kila kitu kinatoka kwa Baba ambaye ni chanzo cha vyote, na kinapitia kwa Yesu ambaye anakigawa kulingana na mapenzi yake.

Kwa hiyo, tukisema kuna Mungu mmoja tu, katika maana hii Mungu huyo ni Mungu Baba peke yake, wala sio Yesu, hapa Yesu ni Mwana wa Mungu mmoja. Lakini ukikutana na Maandiko yanayosema kuwa Yesu ni Mungu, jua kuwa Maandiko hayo yanaonyesha asili ya Uungu wake ambayo aliirithi kutoka kwa Baba yake, na hivyo Yeye ni Mungu kwa sababu ni Mwana wa Mungu, kama wewe ulivyo mwanadamu kwa sababu u mwana wa mwanadamu. Lakini Yesu sio Mungu mmoja tu kama fundisho la utatu linavyofundisha.

1Wkorinto 8:6 “lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo. Bali ujuzi huu haumo ndani ya watu wote;…

Waefeso 4:6 “Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.”

Kwa ajili ya Waadventista: Ellen White anakubali kwamba Yesu sio Mungu Baba, anasema, “Maandiko yanaonyesha wazi wazi uhusiano kati ya Mungu na Kristo, na yanaleta kwenye wazo kama ilivyo wazi Nafsi na Nafsi ya kila mmoja [Waebrania 1:1-5 imenukuuliwa]. Mungu ni Baba wa Kristo; Kristo ni Mwana wa Mungu. Kwa Kristo imetolewa nafasi iliyotukuka. Amefanywa sawa na Baba. Makusudi yote ya Mungu yamefunguliwa kwa Mwana wake.” –(Testimonies for the Church, vol 8, p 268).

Yeye [Kristo] hakuwa Baba lakini ndani yake ulikaa utimilifu wote wa Uungu wazi wazi.” —(E.G. White, Lt8a, July 7, 1890)

“Mtu Kristo Yesu hakuwa Bwana Mungu Mwenyezi, lakini Kristo na Baba ni wamoja.” –(SDA Bible Commentary, vol 5, p 1129).

“Bwana Yesu Kristo, mzaliwa pekee wa Baba, kiukweli ni Mungu katika kutokuwa na ukomo, lakini sio katika nafsi.” –(Ellen G. White, UL 367).

“Umoja ambao upo kati ya Kristo na wanafunzi wake hauharibu nafsi. Wao ni wamoja katika madhumuni, katika mawazo, katika tabia, lakini sio katika nafsi. Ni kwa hivyo ambavyo Mungu na Kristo ni wamoja.” —(E.G. White, 8T 269.4, 1904)

“Mtu mmoja tu katika ulimwengu badala ya Baba anachukuwa jina la Mungu, na huyo ni Mwanawe, Yesu Kristo.” —(J.E. White,Coming King, p. 33)

Je Yohana 1:1 inasema kuwa Yesu ni Mungu?

Yohana 1:1 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”

Huyu Neno si mtu mwingine bali ni Yesu Kristo Mwana wa Mungu Mwenyewe, maana katika Yohana 1 fungu la 14 tunaambiwa kwamba, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Hivyo, huyo Neno sio “neno halisi” kama Yohana 1:14 inavyoweka wazi, bali alikuwa ni “Mwana pekee wa Baba” ambaye alifanyika mwili wa kibinaadamu; yaani, mwili wa dhambi (Rum 8:) kwa njia ya kuzaliwa na bikra Maria ili aweze kuwa na asili moja pamoja nasi na kukaa kwetu ili tuuone utukufu wake kama Mwana pekee aliyetoka kwa Baba. Kabla Yesu hajafanyika Mwili, au kabla hajazaliwa hapa duniani, Yeye alikuwa ni Mwana wa Mungu (Mithali 8:22-25; Yn 3:16), na mwana siku zote hurithi asili, tabia, sifa na jina la baba yake, hivyo, Yesu pia kama Mwana wa Mungu alirithi vitu vyote (Ebr 1:2) pamoja na jina la “Mungu” (Ebr 1:4,8-9). Kwa hiyo, Yesu ni Mungu kwa sababu ni Mwana wa Mungu, kama wewe ulivyo mwanadamu kwa sababu u mwana wa mwanadamu. Na kwa sababu hiyo, Yesu pale kabla hajaja hapa duniani alikuwa ana namna ya Mungu, au alikuwa sawa na Mungu.

Wafilipi 2:5-7 inasema, “Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;”

Kwa hiyo Wafilipi 2:5-6 inasema “hapo mwanzo” Kristo alikuwa na namna ya Mungu, na alikuwa sawa na Mungu. Kwanini? Kwa sababu Kristo ni Mwana halisi wa Mungu, na hivyo alirithi kutoka kwa Baba yake asili, tabia na sifa zote za Uungu. Ndio maana Yohana 1:1 inatuambia kuwa “Naye Neno [Kristo] alikuwa ni Mungu” lakini ili kututhibitishia kwamba Kristo hakuwa Mungu Mwenye, ikaendelea kusema kwamba, “Naye Neno [Kristo, ambaye ni Mungu] alikuwa kwa Mungu.” Hivyo, Kristo hakuwa Mungu Mwenyewe, bali alikuwa kwa Mungu Mwenyewe, lakini kwa sababu ana asili na sifa za Uungu, hivyo naye alikuwa Mungu kwa asili au kwa uwezo, lakini hakuwa Mungu Mwenyewe ambaye ni Baba, Yeye alikuwa ni Mwana wa Mungu. Kwa hakika Yohana 1:14 inathibitisha kwamba, huyo Neno [ambaye ni Kristo] alifanyika mwili akaja kukaa kwetu, nasi tukajua ya kuwa ni “Mwana pekee aliyetoka kwa Baba”. Na Wafilipi 2:5-7 inasema, kufanyika mwili huko, ni pale Kristo alipoamua kuachana na ile namna ya kufanana na Mungu, na akakubali kuchukua namna ya mtumwa ya mfano wa mwanadamu. Hivyo, kama Kristo alikuwa anafanana na Mungu, Yeye hakuwa Mungu Mwenyewe, bali alikuwa Mwana pekee wa Mungu, ambaye amerithi sifa zote za Uungu.

Fundisho la utatu hudai kwamba huyo Neno wa Yohana 1:1 ni “neno halisi” la Mungu Mwenyewe, na hivyo Yesu ni Mungu mmoja yuleyule, ambaye ni mmoja katika watatu, au watatu katika mmoja. Hii haiwezi kuwa kweli, kwa sababu katika Yohana 1:4 tumeambiwa kuwa Yule Neno alikuwa Mwana pekee aliyetoka kwa Baba, harafu Wafilipi 2:5-7 ikathibitisha kwamba, hapo mwanzo Yesu alikuwa na namna ya Mungu, lakini akaja huku na kuchukua namna ya mwanadamu, kitu ambacho kinaonyesha kuwa alikuwa ni mtu halisi mwenye nafsi na sifa kama za Mungu (Ebr 1:3), na hivyo hawezi kuwa “Neno” halisi la Mungu; kwa maana, kama kweli Yesu ni “Neno halisi”, basi hawezi kuwa wa namna ya, au wa kufanana na Mungu, labda mpaka Mungu naye awe “Neno halisi”. Lakini sisi tuliumbwa kwa mfano wa Mungu (Mwa. 1:27) na hivyo Mungu ana mwili (Mt. 5:8), na ili Yesu awe wa namna ya Mungu, lazima awe na mwili; kwa hakika Ebr. 1:3 inasema, Yesu ni mfano halisi wa nafsi ya Mungu; Kwa hiyo, Yeye ana mwili halisi kama Baba yake, na hawezi kuwa “Neno halisi” bali Neno ni jina tu linalotumika kwake kuonyesha sifa zake.

Hata hivyo, “Neno” ni jina tu linalotumika kwa ajili ya Yesu Kristo, wala halimaanishi kwamba Yesu ni Neno halisi kabisa. Kwa mfano; katika Maandiko, Yesu huitwa “Mwana-Kondoo, Je Yesu sasa ni mtoto halisi wa kondoo? Hapana! Pia huitwa “Mzabibu”, Je Yesu sasa ni mti halisi wa mzabibu? Hapana! Pia huitwa “Simba wa Yuda”, Je Yesu sasa ni mnyama halisi ambaye ni simba? Hapana! Pia huitwa “Mkate wa uzima”, Je Yesu sasa ni mkate halisi? Hapana! Hivyo, Yesu sio “Neno” halisi la Mungu, bali majina hayo yote yanaonyesha sifa tu alizonazo Yesu. Kwa mfano jina la “Neno” linamfaa Yesu kwa sababu” Maneno” yote ya Mungu hupitia kwa Yesu kuja kwetu, hivyo Yesu kuitwa “Neno la Mungu” inaonyesha sifa zake, kwa maana Yeye ndiye mwanzo wa kuwapo Maneno yote ya Biblia, lakini chanzo cha Maneno yote ya Biblia ni Mungu Mwenyewe ambaye ni Baba (1Kor 8:6).

Hivyo, Yohana 1:1 inamaanisha kwamba, “Neno alikuwa Mungu” lakini huyo “Neno alikuwa kwa Mungu” na fungu la 14 linasema kwamba, huyo “Neno alikuwa Mwana pekee wa Baba”, Hivyo, Neno alikuwa Mungu kwa sababu Yeye ni Mwana wa Mungu, kama wewe ulivyo mwanadamu kwa sababu u mwana wa mwanadamu. Lakini hii haimaanishi kwamba yule Neno ndiye Mungu mmoja, bali yule Neno ni Mwana wa Mungu mmoja.

Je jina la “Mwokozi” linathibitisha kuwa Yesu na Mungu ni mtu mmoja yuleyule?

Wengi wanadhani kwamba Biblia ikisema, “Mungu Mwokozi” basi inamaanisha Mungu huyo ni Yesu kwa sababu Yesu ndiye Mwokozi wetu. Lakini tunapaswa kuelewa kwamba Kristo na Mungu ni watu wawili tofauti; Mungu ni Baba yake na Kristo, na Kristo ni Mwana wa Mungu. Kristo alirithi vitu vyote kutoka kwa Mungu (Mt 28:18; Ebr. 1:2,4), hivyo chanzo kikuu ambacho kwa hicho wokovu unapatikana ni Mungu Baba, lakini njia pekee ambayo kwa hiyo tunaweza kuupata wokovu huo ni Yesu Kristo. Mtume Paulo katika 1 Wakorinto 8:6 ameonyesha kuwa “Mungu ni mmoja tu ambaye ni Baba, na vitu vyote vinatoka kwake” hivyo, Mungu ni chanzo kikuu cha kupatikana vitu vyote pamoja na wokovu. Lakini pia Mtume Paulo akaendelea kusema kwamba, “yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kupitia Yeye vitu vyote vimekuwapo”, hivyo, Yesu Kristo ni njia ambayo vitu vyote–pamoja na wokovu–vinavyotoka kwa Mungu vinapitia. Kwa hiyo hitimisho ni kwamba, Mungu ni Mwokozi kwa sababu wokovu unatoka kwake, na Yesu ni Mwokozi kwa sababu wokovu unapitia kwake kuja kwetu, hivyo Yesu akitukataa na kwa Mungu tumekataliwa pia, lakini Yesu akitukubali na kwa Mungu tumekubalika pia kwa sababu Yeye ndiyo njia pekee kwetu ya kumfikia Mungu.

Jambo hili hili linatumika kwetu pia, kama tukimkataa Kristo ambaye ni njia ya kumfikia Mungu, pia tunakuwa na hatia ya kumkataa Mungu. Lakini kama tukimkubali Kristo, pia tumemkubali na Mungu (1Yoh 2:22,23). Na hii ndio sababu shetani anajaribu kuleta mafundisho yanayomuondoa Kristo ili injili iwe kazi bure kabisa, na haijalishi ni kwa jinsi gani fundisho hilo linamwondoa Kristo, fundisho linaweza kumuinua Kristo katika nafasi kuu, lakini kama fundisho hilo linahitimisha kwamba Kristo na Baba ni mtu mmoja yule yule tu, kwa hakika hapa Kristo ameondolewa na wokovu haupo kwa sababu Yeye ndiye njia pekee ya kuupata wokovu huo.

Mafungu yafuatayo ni baadhi ya mafungu mengi yanayomwita Mungu jina la “Mwokozi”. Na Je Mungu huyo ni Yesu Kristo au ni Baba wa Yesu Kristo?

1Timotheo 4:10 “kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio.”

Tito 1:3 “akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu;.

Tito 2:10 “wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote.”

Je mafungu hayo yanasema kwamba “Mungu Mwokozi” ni Yesu?

1Timotheo 2:3-5 inasema, “Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;…Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;”

Hapa Mungu ametajwa kama Mwokozi ambaye ni Mungu mmoja, harafu akatajwa na Bwana Yesu kwamba ni Mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, hivyo Yesu sio yule Mungu mmoja Mwokozi, ila Yeye ni mtu mwingine tofauti anayewapatanisha wanadamu na yule Mungu mmoja Mwokozi.

1Timotheo 1:1 “Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu;

Hapa Paulo anamtaja Mungu kama “Mwokozi”, harafu tena anamtaja Yesu Kristo kama mtu mwingine tofauti na huyo Mungu Mwokozi, hii inaonyesha kwamba jina la “Mwokozi” halitumiki kwa Yesu peke yake, bali linatumika na kwa Mungu ambaye ni Baba wa Yesu.

Luka 1:47 “Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;

Tito 3:4 “Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;”

Huyu “Mwokozi wetu Mungu” ambaye upendo wake umefunuliwa kwetu, kwa hakika ni Mungu Baba na wala si Kristo; kwa maana “Yeye aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwana wake wa pekee ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” Yn. 3:16. Ukisoma katika Tito 3 fungu la 6 linathibitisha kuwa huyu Mungu wetu Mwokozi “alitumwagia [Roho Mtakatifu] kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu;” Hivyo, hapa utaona “Mungu wetu Mwokozi” ni mtu mmoja anayetumwagia Roho wake kupitia “Yesu Kristo Mwokozi wetu” ambaye naye ni mtu mwingine tofauti, kwa hiyo jina la “Mwokozi” linatumika kwa wote wawili, kwa Mungu ambaye ni Baba, na kwa Yesu Kristo Mwanawe. Hivyo, kudai kwamba kila fungu linalosema “Mungu Mwokozi” basi linamaanisha Mungu huyo ni Yesu eti kwa sababu Yesu ni Mwokozi, hili litakuwa ni kosa; kwa maana Maandiko yanaeleza wazi kwamba, “Baba ni Mwokozi” na “Yesu ni Mwokozi”. Baba ndiye chanzo cha wokovu, na Yesu ndiye njia ya wokovu.

Sasa kama Mungu ni Mwokozi, na Yesu ni Mwokozi, jumla Waokozi wawili kwanini tena Maandiko yanasema…

Isaya 43:11 “Mimi, naam, mimi, ni Bwana, zaidi yangu mimi hapana mwokozi.”

Hosea 13:4 “Lakini mimi ni Bwana, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna Mwokozi.”

Kusema kwamba “Mwokozi ni mmoja tu” neno hili linamaana mbili tofauti. Katika maana ya kwanza Mungu Baba ni Mwokozi, na kwa kuwa Yeye ni yote katika wote (1Kor. 15:28), naye ndiye chanzo kikuu cha wokovu wetu wote (1Kor. 8:6), na bila Yeye kwa kweli wokovu usingekuwepo, na hivyo Yeye ni Mwokozi peke yake katika maana hii ya kwanza.

Lakini katika maana nyingine Yesu ni Mwokozi, na tafadhari kumbuka kwamba Yesu sio chanzo kikuu cha wokovu, bali Yeye ni njia pekee ya wokovu. Yesu Mwenyewe katika Yohana 14:6 anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Kwa hiyo hakuna mtu ye yote anayeweza kuokolewa kama asipopitia kwa Yesu, na hivyo katika maana hii Yesu ni Mwokozi peke yake na hakuna mwingine, lakini hii haimaanishi kwamba Baba sio Mwokozi, Yeye ni Mwokozi na tena ndiye chanzo cha wokovu huo unatufikia kwa njia ya Yesu. Lakini Yesu anakuwa Mwokozi pekee kwa ile maana ya kwamba hatuwezi kuokolewa kama tusipopitia kwake.

Na katika maana ya nyongeza ni kwamba, Yesu ni Mwokozi pekee na hakuna mwingine katika dunia nzima; Kwa sababu Yeye ndiye njia pekee na bila Yeye hakuna wokovu kwetu, Yeye ni Mpatanishi (1Tim. 2:5) wetu anayerudisha uhusiano kati yetu sisi na Mungu.

Hitimisho

Katika hitimisho letu ni kwamba, Yesu ni Mungu kwa sababu ni Mwana wa Mungu. Hivyo, kwa asili ana sifa zote za kiuungu alizopata kwa njia ya kurithi kutoka kwa Baba yake. Licha ya kurithi asili ya uungu, lakini Yeye kama Mwana amerithi na jina la Baba yake, jina lililotukuka kupita la malaika (Ebr. 1:4). Yesu na Baba ni watu wawili tofauti, Mungu ni mmoja tu aliye Baba, Yesu ni Mungu tu kwa asili, uwezo, sifa, tabia, na kutokuwa na ukomo; lakini Yeye sio Mungu katika nafsi ya Mungu Mwenyewe. Yeye ni, na anapaswa kujulikana kama Mwana halisi wa Mungu aliye na sifa za kiuungu kwa njia ya kurithi.

Angalia pia…

  • Je Yesu Kristo ni Mungu Baba?
  • Published by JacksonSL

    My name is Jackson A Kayanda (Full name: Jackson Augustine Kayanda), born on 17th January 1995 at Samina Geita in Tanzania. Went to school for pre and first class primary standard education at Shule ya Msingi Mpomvu in Mtakuja ward in the years 2001 and 2002. After there, I moved to Shule ya Msingi Nyakamwaga in Geita where I spent my final six classes in the years 2003 to 2008. In 2012, I attended a college for auto mechanics technical courses at Kirumba Technical Training Centre (KTTC) where I won a highest Certificate level (grade one) able to perform auto mechanics engineering in both theory and practical works. I'm very interested in reading and writing, this is why I launched Sabbath Light for the good, read to share inspirational facts and ready to receive corrections either. I stay calm in Christ Jesus!