Je Mitume waliunza Sabato ya Jumamosi au Jumapili? Biblia na Historia: Sehemu ya 1


Imedaiwa miongoni mwa wajumapili kwamba Yesu alipofufuka siku ya Jumapili, na Roho Mtakatifu aliposhuka siku ya Jumapili katika Pentekoste, kwa kitendo hicho Yesu aliitakasa jumapili ili watu wake badala ya kutunza Jumamosi waanze kutunza Jumapili. Lakini kama ukirudi katika Maandiko na kuangalia kwa makini, hautaona mahali popote ambapo Yesu Mwenyewe au mtakatifu yeyote amesema kwamba Jumapili ilitakaswa na kubarikiwa. Nataka kuvuta usikivu wako tuchunguze kwa makini katika Biblia ili tuone ni siku gani ambayo Yesu alitakasa. Na Je Yesu alitakasa Jumapili?


Ushahidi katika vitabu vya Injili

Katika Agano Jipya siku ya kwanza ya juma imetajwa mara 8 tu, na mara zote haijasemwa popote kwamba imetakaswa au kwamba Mungu aliagiza watu watunze siku hiyo.

Katika Kitabu cha Mathayo siku ya kwanza ya juma imetajwa mara moja ikihusiana na ufufuo wa Yesu,
na hakuna ibada iliyofanyika siku hiyo, bali Sabato ilipoisha ndipo Mariamu siku ya jumapili alienda kaburini na akakuta Yesu amekwishafufuka.

Mathayo 28:1 “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.”

Tukio hili hili limeandikwa pia katika Injili nyingine zote tatu kama ifuatavyo:

Marko 16:1-2 “Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. 2 Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;”

Angalia walisubiri Sabato ikaisha jioni, ndipo wakanunua manukato ili jumapili asubuhi wakampake Yesu kaburini.

Yohana 20:1 “Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alifajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini.”

Marko 16:9-11″ Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba. 10 Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia. 11 Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki”

Yesu aliipomtokea Mariamu Magdarene siku ya jumapili, Alimwambia “enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. 18 Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.” Yohana 20:17-18. Mpaka Jumapili hiyo aliyofufuka Yesu ilipita, wala Yesu Mwenyewe hakusema, wala hakumwagiza mtu yeyote kwamba kwa sababu amefufuka jumapili basi ameitakasa jumapili na watu wake watunze jumapili badala ya jumamosi.

Tena katika jumapili hiyo ya ufufuo Yesu aliwatokea wanafunzi wake jumapili jioni wamekusanyika kwa hofu ya Wayahudi.

Yohana 20:19-20 “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. 20 Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.”

Hapa Yesu alipowatokea wanafunzi wake ilikuwa ni Jumapili Jioni na jumatatu ndiyo ilikuwa inaanza kuingia, kama Yesu angekuwa na nia ya kuachana na Sabato ya kiyahudi, na kwamba alikuwa ameitakasa jumapili, hapa ndipo alikuwa na nafasi ya kuwaeleza wanafunzi wake. Lakini ukisoma maneno aliyowaambia siku hiyo katika Yohana 20:19-23, na Luka 24:44-49 utaona kuwa hakuna mahali popote alipowaambia kwamba sasa Jumapili nimeitakasa.

Tukihesabu siku nane mbele kutoka jumapili hiyo tunafika katika Jumapili nyingine ambapo Yesu aliwatokea wanafunzi wake tena.

Yohana 20:26 “Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu.”

Milango ilikuwa imefungwa kwa sababu ya hofu ya Wayahudi, na wakati huu wanafunzi wote walikuwepo mahali pamoja, pamoja na Tomaso ambaye pale nyuma hakuwepo. Yesu aliwatokea kwa sababu ya Tomaso ambaye alikuwa hataki kuamini kwamba Bwana amefufuka, na sasa Yesu alishughulika na Tomaso ili apate kuamini. Tena hapa Yesu alikuwa na nafasi ya kuwaambia wanafunzi kwamba ameitakasa Jumapili, lakini katika mazungumzo yake yote na Tomaso siku hiyo hakusema popote kwamba ameitakasa Jumapili, wala hakuagiza amri yoyote kuhusu kupumzika siku ya Jumapili.

Yesu mara kwa mara aliwatokea wanafunzi wake, aliwatokea wanafunzi wawili ambao walikuwa wakielekea kijiji kinachoitwa Emau na akazungumza nao “Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.” (Luka 24:27). Hata hivyo hakusema popote kwamba sasa ameitakasa Jumapili. Wanafunzi hao wawili walirudi kuwapasha habari wale kumi na mmoja kuhusu jambo hilo, tena Yesu akawatoke mara nyingine wakiwa wote na wale kumi na mmoja (Luka 24:36-49), lakini bado hakusema neno lolote kwamba ameitakasa Jumapili. Tukio hili ni lilelile kama la Yohana 21:1-23, ambapo Yesu akimwambia Petro kwamba “Lisha kondoo wangu” (21:17), lakini bado hakuwaambia popote kwamba ameitakasa Jumapili.

Kwa mtu yeyote ambaye ana akili timamu itakuwa ni vigumu sana kuamini kwamba Yesu aliitakasa Jumapili wakati wa kufufuka kwake, na tayari hadi kupaa kwake bado yuko kimya hasemi popote kwamba nimeitakasa Jumapili. Ni kitu ambacho hakiwezekani Yesu kuitakasa jumapili, harafu akakaa kimya siku nyingi namna hiyo asiwaambie wanafunzi wake jambo hilo. Mpaka hapa ushahidi wa vitabu vya Injili vyote vinne viko kimya na havisemi popote kwamba Yesu aliitakasa Jumapili. Vitabu vinne viliandikwa miaka 40 baada ya Yesu kupaa mbinguni, na tayari waandishi wake hawasemi popote kuhusu ibada ya Jumapili.


Sabato ya kwanza baada ya Yesu kupaa.

Tunavuka kutoka vitabu vinne vya Injili hadi kitabu cha Luka cha matendo ya mitume ambacho kinasemekana kiliandikwa miaka 40 au 50 baada ya kupaa kwa Yesu. Hapa ushahidi wa kwanza kabisa tunaoupata ni kwamba, baada ya Yesu kupaa mbinguni mitume walirudi Yerusalemu kusubiri ahadi ya Roho Mtakatifu, na sabato ilipofika iliwakuta wako Yerusalemu, wakaingia orofani walimokuwa wakiishi kina Petro, wakafanya ibada kama ilivyo kawaida kila sabato.

“Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.” Matendo 1:12

Walipofika Yerusalemu, yapata watu mia na ishirini walipanda orofani, walipokuwa wakikaa kina Petro kwa ajili ya kusali, siku hiyo ilikuwa ni siku ya sabato, na Biblia inasema.

“Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.” Matendo 1:14

Katika siku hiyo hiyo ya sabato mtume Petro alisimama akahubiri Injili ya Yesu mbele ya wale watu 120 (angalia Mdo 1:15-20), tena sabato hiyo hiyo walipiga kura na kumchagua Mathiya mahali pa Yuda Iskariote (angalia Mdo 1:21-26). Hii inathibitisha kuwa baada tu ya Yesu kupaa, sabato iliyofuata mitume waliitunza kama ilivyo kawaida ya siku zote. Na siku iliyofuata ilikuwa ni Jumapili siku ya Pentekoste, ambayo tunaelekea kuijadili.


Siku Ya Pentekoste Jumapili.

Baada ya sabato waliyosali mitume kuisha kesho yake ilikuwa ni sivan 6 siku ya Pentekoste, ambayo kwa mzunguko wa mwaka huo iliangukia Jumapili.

Matendo 2:1-4 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. 2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. 3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

Mitume walijua kwamba sivan 6 ni siku ya Pentekoste hivyo wasingetoka kwenda popote kama sheria ya Musa inavyoagiza, walikaa pamoja kwa ajili ya pentekoste, na Mungu akashusha Roho Mtakatifu ili kuitimiliza pentenkoste.

Wengi wamekuja kuamini kwamba siku ya pentekoste ndiyo sababu kuu ya ibada ya hadhara kuhamishiwa Jumapili, lakini hii inatokana na uelewa mdogo au kutokuelewa kabisa nini maana ya Pentekoste. Pentekoste inamaanisha “kuhesabu hamsini”, Mungu alikuwa amewaagiza wana wa Israeli kuhesabu siku hamsini tangu 16 nisani hadi 6 Sivan, Pentekoste siku zote huangukia katika siku ya 6 ya mwezi wa tatu wa kiyahudi unaoitwa Sivan, Sivan 6 inaweza kuangukia katika siku ya wiki yoyote ile, iwe ni jumapili, jumamosi, jumatatu au ijumaa, kulingana na mzunguko wa mwaka ulivyoenda.

Katika Pentekoste Mungu haangalii siku ya wiki wala juma, haangalii jumapili wala jumamosi, bali anaangalia tarehe 6 ya mwezi wa tatu Sivan. Katika kipindi cha mitume Sivan 6 iliangukia jumapili, lakini pia ingeweza kuangukia jumatatu au jumamosi kulingana na mzunguko wa mwaka ulivyo. Kulingana na Walawi 23:16-19 kila ifikapo Pentekoste zingetolewa “sadaka za amani” na “sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto”, Hii ingewakilisha vizuri kushuka kwa Roho Mtakatifu kama ubatizo wa moto katika Sivan 6 ambayo ni pentekoste.

Sivani 6 inaweza kuangukia katika juma lolote, haijalishi ni jumapili, jumamosi, au jumatatu. Hivyo kutumia siku ya Pentekoste ili kufundisha watu kwamba ibada ya hadhara ilihamishiwa jumapili ni kwenda kinyume na utaratibu wa Mungu katika mpangilio wa “siku za sikukuu” alizowapa wana wa Israeli.

Hata hivyo, kama Pentekoste ndiyo sababu ya wewe kwenda kanisani jumapili, inakubidi uitendee haki kwa kuhesabu kwanza siku hamsini ndipo uende kanisani. Vinginevyo Pentekoste haihusiani na jumapili kwa jinsi yoyote ile, Pentekoste ilitimia kama Mungu alivyokuwa ameipangilia, Pentekoste ilihusiana na kutimia kwa ahadi ya Roho Mtakatifu na sio siku ya kusali ibada ya hadhara.

Baadhi wanaweza kudhani kwamba kwa sababu pentekoste hiyo Jumapili mitume walikuwa wako mahali pamoja, hivyo Sabato ilikuwa imehamishiwa siku ya Jumapili. Lakini haiungi mkono swala hili hata kidogo; kwa kuwa ilikuwa ni kawaida ya mitume kusali na kumhubiri Yesu kila siku, na hata hivyo siku ya Sabato walipumzika, si kupumzika katika kuhubiri Injili, bali kupumzika kutoka katika kazi zao wenyewe kama sheria inavyogiza.

Luka 24:51-53 “Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni. 52 Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. 53 Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.”

Matendo 5:42 “Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.”

Baada ya kupaa kwa Yesu mitume walikuwa kila siku wanahubiri Injili, na hivyo jumapili iliyofuata hata kama ingekuwa sio pentekoste, lazima ingewakuta wakiwa pamoja. Lakini hii haimaanishi kwamba sabato ilihamishiwa siku ya jumapili; kwa maana historia iliyofuata inathibitisha ukweli huu, jinsi walivyoendelea kutunza Sabato, na walifanya kazi siku ya jumapili kama utakavyokuja kuona huko mbele.


Kukutana Kwa Simon Petro na Simon mchawi.

Sasa tunaruka hadi sura ya 8 ya kitabu cha Matendo ya mitume ambapo tunaona Mitume Petro na Yohana walitumwa kwenda Samaria kuwaombea watu waliobatizwa wapokee Roho Mtakatifu

Matendo 8:14-15 “Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; 15 ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;”

Petro alipofika Samaria alikutana na Simoni Mchawi ambaye naye alikuwa amebatizwa, na alipoona kuwa Petro anawawekea mkono watu nao wanapokea Roho Mtakatifu, Simon Mchawi akatamani kununua karama hiyo, ndipo mtume Petro akamkemea (angalia aya 8:18-23). Sasa baadhi ya wanahistoria wa mapema hudai kwamba jambo hilo lilitokea katika siku ya Sabato, na kwamba mtume Petro na wakristo wa mahali hapo walikuwa na desturi ya kufunga kila siku ya Sabato.

“Uandishi wa baadaye unatangaza kwamba vita. . .[ya Simon] pamoja na Petro ilitokea siku ya Sabato ambapo waaminifu walikuwa wanafanya “proseuche” (yaan, mkutano wa sinagogi) na kufunga hasa kwa sababu ya mwalimu wao Simon (Glycas, “Annales,” ed Bonn. , i. 236, 439). Wakati ni kweli kwamba Wakristo walikuwa tayari wanatofautiana kidogo na wenzao Wayahudi, na kwamba “waaminifu” inaweza sawa vizuri kuwa Wakristo, lakini kufunga (Warumi waliamini kuwa Wayahudi walifunga siku ya Sabato), kwa mfano, kuacha kufanya kazi, ni kwa kawaida ya Kiyahudi.” —(Jewish Encyclopedia, “Simon Magus“)

John Cassian akizungumzia kuhusu ufungaji wa Waroma katika siku ya Sabato, anatupa ushahidi kwamba Mtume Petro kabla ya kukutana na Simon Mchawi, alifunga siku ya Sabato. Anasema:

“Jinsi gani jambo hili kwamba walifunga siku ya Sabato katika mji. Lakini baadhi ya watu katika baadhi ya nchi za Magharibi na hasa katika mji, bila kujua sababu ya upendeleo huu, wanafikiri kwamba jambo la kuacha kufunga halipaswi kabisa kuruhusiwa siku ya Sabato, kwa sababu wanasema kwamba katika siku hii Mtume Petro alifunga kabla ya kukutana na Simoni [mchawi]. Lakini kutokana na hili ni wazi kabisa kwamba [Mtume Petro] alifanya hivyo si kwa mujibu wa kanuni ya kisheria, bali kwa njia ya mahitaji ya mapambano mabaya yaliyomkabiri.” —(Philip Schaff, Nicene and Post Nicene Fathers, Series II, Volume 11, Chapter X, Page 218)

Katika “Tanibihi” ya maelezo hayo juu inasema: “Kufunga siku ya Jumamosi kuliadhimishwa huko Roma, katika siku za mwanzo kabisa, jambo hili likionwa na Tertullian, ambaye anaonekana kupendekeza kwamba ilitokana na urefusho wa kufunga kwa Ijumaa (On Fasting, c. xiv). Lakini linaonekana kuwa karibu la pekee huko Roma, na huko Milan, katika muda wa S. Ambrose, desturi za Mashariki zilishinda. Angalia barua muhimu ya Augustine kwa Casulanus (Ep. xxxvi.), ambapo jambo lote la utofauti wa matumizi ya suala hili limejadiliwa kikamilifu.”

Hivyo kama ushahidi huu ni wa kweli, tunauhakika kwamba Petro na Wakristo wote wa kipindi hicho walitunza Sabato, na hata baadhi walifunga siku ya Sabato. Na ushahidi huu ni wa kweli; kwa sababu Waroma wengi wa hapo zamani waliamini kuwa mtume Petro alifunga katika siku ya Sabato kabla ya kukutana na Simoni Mchawi.


Paulo ahutubu huko Troa siku ya Jumapili. Je hii inamaanisha mitume walitunza Jumapili kitakatifu?

Matendo 20:7 “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.”

Katika Biblia siku huanza jioni na kuisha jioni, hivyo hapa walikuwa wamekutana Jumamosi siku ya Sabato ili kufanya ibada, na Sabato ilipoisha wakati wa jioni, ndipo Jumapili, siku ya kwanza ya juma ikaingia. Kwa sababu mtume Paulo alitaka kusafiri kesho yake asubuhi—neno “siku ya pili yake” la kigiriki ni: ἐπαύριον (epaurion)—na linamaanisha pia asubuhi inayofuata, na kwa kuwa walikuwa wanamega mkate, hivyo ikawachukua muda hadi usiku wa manane. Kesho yake asubuhi ilikuwa ni jumapili, na hawakufanya ibada yoyote, bali Mtume Paulo alisafiri Jumapili hiyo asubuhi.

Hapa Mtume Paulo alisubiri mpaka Sabato ya kiyahudi ikaisha wakati wa jioni, na ilipoingia Jumapili, usiku, akawahutubu watu wa Troa ili kuwaaga kwamba kesho yake asubuhi angeondoka. Swali linabaki kwamba, kama jumapili ilikuwa imetakaswa na mitume walikuwa tayari wanafanya ibada ya hadhara katika siku hiyo kama baadhi ya watu wanavyodhani. Ingewezekanaje mtume Paulo kuendesha ibada Jumapili usiku harafu kesho yake Jumapili asubuhi badala ya kuendesha ibada yeye akaitumia kusafiri? Lakini utasema kwamba walikuwa wakimega mkate Jumapili hiyo usiku, ndiyo, mkate walimega siku zote, na sio jumapili usiku tu. Matendo 2:42,46 inasema “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. . . .46 Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe.”

Au kama ukisema kwamba Paulo aliwahutubu, ndiyo aliwahubu, wao walihutubu kila siku, na walidumu katika mafundisho ya mitume kila siku, kama sisi leo tunavyofanya ibada majumani mwetu usiku kila siku. Luka 24:53 inasema, “Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.” Paulo “aliwahutubu akiazimu kusafiri kesho yake asubuhi”; na hivyo alikuwa akiagana nao, na kuwasihi kwa machozi kwamba wadumu katika imani ili ibilisi asiwachukue katika mtego wake, kitu kilichomchukua muda mrefu kukikamilisha hadi usiku wa manane; na kesho yake Jumapili asubuhi ilipofika Paulo akaondoka kwenda safari yake. Matendo 20:11 inasema, “Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake.” Alienda zake jumapili hiyo asubuhi.

Kutumia Matendo 20:7 ili kumshawishi mtu kwamba mitume waliachana na Sabato, badala yake wakatunza Jumapili, si kutumia Maandiko kwa uaminifu. Kesho yake Jumapili asubuhi, Paulo alisafiri na hakufanya ibada yoyote. Hivyo makanisa yote yanayosali ibada ya hadhara siku ya Jumapili kwa kisingizio cha fungu la Matendo 20:7, ili yalitendee haki fungu hilo, yanapaswa kufanya ibada zao kila Jumapili usiku, na sio asubuhi au mchana.


Je Wakorinto walitunza Jumapili au Jumamosi?

1 Wakorinto 16:2 “Siku ya kwanza ya juma [Jumapili] kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;”

Je hii inamaanisha kwamba huko Korinto watu walifanya ibada ya hadhara siku ya Jumapili? Kwa hakika hapana! Paulo aliwaagiza Wakorinto vilevile kama alivyokuwa amewaagiza Wagalatia (1 Kor. 16:1) kwamba siku ya jumapili watunze kiasi cha pesa kulingana na kila mtu alivyobarikiwa, ili Paulo atakapoenda Korinto pesa hizo ziwe tayari, na isiwepo haja ya kuchagiza tena. Pesa hizo zilikuwa ni mchango kwa ajili ya watakatifu waliozihitaji huko Yerusalemu, na wakati ambapo Paulo angelifika huko Korinto, angelizikuta zikiwa tayari naye angelizituma kwenda Yerusalemu ili kufanikisha mahitaji hayo (1 Kor. 16:3). Hivyo pesa hizo zilikuwa sio dhaka, wala sadaka, bali ni changizo tu, ambalo wakati Paulo angefika Korinto angezituma zote kwenda Yerusalemu na changizo hilo lingefikia mwisho.

Kwa sababu Wakristo waliruhusiwa kufanya kazi siku ya Jumapili, hivyo kiasi cha pesa ambacho wangebarikiwa na Mungu kukipata Jumapili hiyo, wangekiweka akiba kwa ajili ya mchango uliohitajika huko Yerusalemu. Hii isingewezekana kufanywa siku ya Sabato, Jumamosi; kwa maana hamna pesa yoyote inayopatikana siku hiyo kwa kuwa Wakristo wote hawakufanya kazi Jumamosi.

Wale wanaotumia fungu hili kudai kwamba linathibitisha kwamba Wakorinto walifanya ibada ya hadhara siku ya Jumapili, hii sio kweli. Na ili kuvunja madai haya ngoja tuangalie kama kanisa la Korinto walitunza Sabato au Jumapili. Wengi wamedanganywa kwa sababu wanaposoma fungu ambalo kwanza halisemi wazi wazi kwamba kulikuwa na ibada ya Jumapili hapo, wanakuwa wavivu kuangalia nini zaidi Biblia inasema ili kuthibitisha msimamo wao. Paulo yeye mwenyewe ndiye alianzisha kanisa la huko Korinto, Je Paulo alianzisha kanisa la kutunza Jumapili au la kutunza Jumamosi, Sabato? Kanisa la Wakorinto walitunza Sabato na sio Jumapili.

Matendo 18:1 “Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.”

Je Paulo alipofika Korintho alitunza Jumamosi, Sabato, au Jumapili? Paulo alipofika Korintho alikutana na Myahudi mmoja anayeitwa Akila, pamoja na Prisila mkewe, hao pamoja na Paulo walikuwa mafundi wa kushona hema, na Paulo akakaa pamoja nao wakafanya kazi ya kushona mahema (Mdo 18:2). Sasa wakati Paulo anaishi huko Korinto na kufanya kazi ya kushona mahema, je alitunza Sabato, Jumamosi, au alitunza Jumapili?

Matendo 18:4 “Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.”

Paulo akiwa Korintho akifanya kazi ya kushona mahema, kila sabato alihudhuria kwenye sinagogi kutoa hoja zake ili awaongoe Wayahudi na watu wa mataifa pia. Kwanini hakufanya hivyo kila Jumapili kama Wakorinto walitunza Jumapili?

Baada ya Paulo kufarakana na Wayahudi, alienda katika nyumba ya mtu mmoja aliyekuwa akiishi karibu na sinagogi, na Wakorinto wengi wakaamini mahubiri yake. Paulo akakaa huko Korinto muda wa mwaka na miezi 6.

Matendo 18:11 “Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu.”

Katika muda huo Paulo alitunza Sabato 72 huko Korintho, na hakuna shaka kabisa kwamba Paulo wakati huo alianzisha rasmi kanisa la kutunza Sabato huko Korintho, na hakuna sehemu yoyote inayosema kwamba hapo Paulo alitunza Jumapili. Ni kweli kwamba Paulo akiwa huko Korintho alikataa sheria za kafara na sikukuu za kiyahudi za miandamo ya mwezi; yaan, sikukuu za kuadhimishwa kwa kufuata tarehe; kwa jina lingine zinaitwa “sabato za mwaka” ambazo zilitokea kwa mwaka mara moja tu katika mwezi ulioteuliwa, lakini alitunza Sabato ya wiki ambayo haihusiani na tarehe wala mwandamo wa mwezi na kanisa aliloanzisha huko ni la watunza Sabato. Hivyo wakati mtu anapotumia 1 Korintho 16:2 kudai kuwa Wakorinto walitunza Jumapili, madai yake si kweli, kwani Wakorinto walitunza Sabato.


Paulo aanzisha kanisa la watunza Sabato huko Antiokia!

Matendo 13:1 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli [ambaye ni Paulo].”

Kumbuka kuwa kanisa hili lililopo Antioki walikuwa ni watunza sabato kama tunavyoenda kuona hivi karibuni. Kanisa hili walifanya ibada na kufunga na kuomba, na Roho Mtakatifu akawaagiza kwamba wamtengee Paulo na Barnaba kwa ajili ya kazi ya kuhubiri Injiri. Ndipo kanisa hili likaweka mikono juu ya Paulo na Barnaba na kuwaacha waende zao (Mdo 13:3).

Paulo na Barnaba wakapelekwa au wakaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda Seleukia, Kipro, na katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi. Kisha wakenda Pafo, kutoka hapo waekaelekea Perge, na kutoka hapo wakarudi tena Antiokia na siku ya Sabato wakaingia katika Sinagogi.

Matendo 13:14 “Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi.”

Basi, wakuu wa sinagogi wakawauliza ikiwa wana neno la kusema, ndipo Paulo akasimama na kuanza kuwahubiri habari za Yesu kwamba ndiye Kristo, akithibitisha kwa maandiko kutoka katika Agano la Kale na kuonyesha utimilifu wake katika Agano Jipya. Na alipomaliza wakamuomba awahubiri tena sabato ifuatayo.

Matendo 13:42 “Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili.”

Na watu wengi wakawafuata Paulo na Barnaba. Matendo 13:43 “Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu.” Tena Sabato iliyofuata Paulo akaenda kuwahubiri.

Matendo 13:44 “Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.”

Katika Sabato ya pili watu wote wa mataifa pamoja na Wayahudi karibu mji wote walikusanyika kusikia neno la Mungu. Inawezekanaje Paulo kusubiri hadi Sabato ya pili, ikiwa Sabato ilitanguka. Kwanini asingesema wazi kwamba sitakuja sabato ya pili bali ntakuja Jumapili? Baada ya Paulo kuhubiri Jumamosi ile, kesho yake Jumapili alikuwa na nafasi ya kuhubiri, lakini ni kwanini hakuhubiri Jumpili bali alisubiri hata Sabato ifuatayo ndipo akaenda kuhubiri? Na ni kwanini aliwahubiri mambo yote hayo lakini hakusema popote kwamba na Sabato imetanguka? Je Paulo alipojipatia watu wa mataifa karibu mji wote siku ile, aliwaambia kwamba hampaswi kutunza sabato ya kwenye amri kumi? Hapana!

Matendo 13:48-49 “Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. 49 Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.”

Baadaye Wayahudi wakaleta fitina juu ya Paulo na Barnaba, na watu walioamini. Basi, Paulo na Barnaba wakakung’uta mavumbi kisha wakaenda Ikonio (Mdo 13:51), wakawaacha pale “wanafunzi [walioamini] wamejaa furaha na Roho Mtakatifu.” (Mdo 13:52). Paulo hakuwaagiza mahali popote kwamba waachie kutunza Sabato, ni hakika kwamba kanisa alilolianzisha hapo katika siku ya Sabato hiyo ya pili ambapo mji wote ulikusanyika kumsikiliza, liliendelea kuwa kanisa la watunza Sabato waliojaa furaha na Roho Mtakatifu, waliendelea kufuata desturi ya Paulo mwenyewe; nayo ni amri ya Mungu. Kanisa la Antiokia katika kipindi chote cha mitume walikuwa ni watunza Sabato.


Endelea: Sehemu ya 02


Published by JacksonSL

My name is Jackson A Kayanda (Full name: Jackson Augustine Kayanda), born on 17th January 1995 at Samina Geita in Tanzania. Went to school for pre and first class primary standard education at Shule ya Msingi Mpomvu in Mtakuja ward in the years 2001 and 2002. After there, I moved to Shule ya Msingi Nyakamwaga in Geita where I spent my final six classes in the years 2003 to 2008. In 2012, I attended a college for auto mechanics technical courses at Kirumba Technical Training Centre (KTTC) where I won a highest Certificate level (grade one) able to perform auto mechanics engineering in both theory and practical works. I'm very interested in reading and writing, this is why I launched Sabbath Light for the good, read to share inspirational facts and ready to receive corrections either. I stay calm in Christ Jesus!